×

Injili ni neno ambalo yawezekana  sisi sote tumelisikia mara nyingi katika maisha yetu ya kila siku ya Ukristo wetu. Hata unapomueleza Mkristo mwingine yeyote atakwambia kuwa injili ni “Habari njema”. Na hata unapomueleza Mkristo huyo  hizo habari njema anaweza kufikiri vizuri kwa kujiuliza swali Je, ni habari  zipi hizo? Na hata akaweza kukupa majibu tofauti tofauti ya kukushangaza sana!

Msomi, na Profesa wa Agano Jipya katika chuo theolojia, David Seccombe anaandika akisema “Injili ni muhimu kwa sababu watu wanaishi katika mwili na injili  ndiyo inayotupa uzima, na ni pekee inayotupa uzima.”

Injili ni muhimu kwa sababu watu wanaishi katika mwili na injili  ndiyo inayotupa uzima, na ni pekee inayotupa uzima.

Tukiangalia kiasili injili ni neno lenye asili ya lugha ya kigiriki, evangelion, lililotafsiriwa habari njema yaani habari ya Yesu Kristo; kufa  kwake, kufufuka kwake, kupaa kwake, na hata atakaporudi tena mara ya pili. Neno hili injili pia limetumika kuhusu vitabu vinavyoelezea maisha na mafundisho ya Yesu, ambayo ni injili ya Mathayo, Marko, Luka na Yohana. Vitabu vitatu vya kwanza vya injili vinafanana kwa kiasi kikubwa sana katika mpangilio, habari na maneno yenyewe. 

Wengine wanaweza kutafsiri kuwa injili ni namna ya kuangalia ukweli wa Kikristo, katika hili lililo la msingi zaidi ni umuhimu wa Injili katika dunia yetu hii kwa nyakati zote. Yesu Kristo aliwaamuru wanafunzi wake waende kuihubiri injili duniani kote mpaka miisho ya nchi. Na hili limeendelea kuwako hata hivi leo hii.

“Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote,kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mathayo 24:14)

Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote,kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mathayo 24:14)

“Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyoyawaamuru ninyi na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:16-20)

Hii inatupa sisi sote ujumbe wa Ukristo kuwa unaweza ukaeleweka, kufafanuliwa, nakuelezeka kiurahisi.

Kulingana na Mtume Paulo, “Injili” ni chombo ambacho Mungu anakitumia katika kuwaokoa wanadamu” (Warumi 1:16, 1Wakorintho 1:17-25)

Kwa ufupisho, injili ni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote, juu ya Yesu Kristo, (Luka 2:10) 

“Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha itakayokuwa kwa watu wote”

 Kwamba ni mwana wa Mungu.(Yohana 1:1, 18, 20:28, Rum 9:5, Kol 1:15-19.2:9. Tito 2:13, Waebrania 8:1, Yohana 5:20, 2Petro 1:1)  na alitwaa ubinadamu kwa ajili yetu sote, Mathayo 1:23,Luka 2:10-11,Yohana 1:14, 1Tim 3:16, Fil 2:7-8, 1Petro 1:20, 1Yohana 1:1-2) na kwamba alikufa (1Kor 15:3b, Rum 3:25-26, 1Petro 2:24) akazikwa (1Kor 13:4a) na alifufuka (Mathayo 28:1-10, Mk.16:1-18, Luka 24:1-12, Yohana 20:1-10, Mdo 2:24-32, 1Kor 2:9-11

Kwa nini injili ni muhimu?

  • Inaleta imani: “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo na ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Waebrania 11:1) Imani huja kwa kusikia na kusikia Neno la Mungu” Injili ni huduma ya Roho Mtakatifu kwa kutuletea watu wa ulimwengu wokovu. Injili ni “uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye…”
  • Injili ina umuhimu wa kuimarisha imani, kwa imani tunampokea Kristo na kila faida yote katika kuoshwa na kutakaswa, injili inapaswa kuhubiriwa kwa watu wote, na sio tu wasioamini, bali kwa wale wanaoamini pia. (warumi 1:15) “Lakini kwa upande wangu mimi niko tayari kuihubiri injili hata kwenu ninyi mnaokaa Rumi”
  • Injili inatupa unyenyekevu na pia inamwinua Bwana Mungu wetu: Katika kanisa hakuna kitu chochote chenye utukufu kama huduma ya kuihubiri injili ya Yesu Kristo ( Warumi 11:36,16:27, Gal 1:3-5. Waefeso 1:3-14) Lazima injili iwe ndio mkazo mkuu na ihubiriwe kwa ufasaha na Kweli yote.

Katika wazo la injili ya kweli, hii ni habari njema kwamba Mungu anatuokoa sisi tulio wenye dhambi. Dhambi zimetutenganisha na Mungu bila tumaini la kurekebisha hali hiyo. Lakini Mungu ametoa njia ya ukombozi wa mwanadamu katika kufa na kufufuka kwa Mwokozi Yesu Kristo. Katika anguko la mwanadamu pale kwenye bustani ya Edeni, (Mwanzo 3:6), kila sehemu ya mwanadamu: mawazo yake, mapenzi yake, hisia zake na mwili wake wote yaliharibiwa na dhambi. Kwa sababu ya asili ya dhambi ya mwanadamu, hawezi kumtafuta Mungu, hana hamu ya kuja kwa Mungu (Warumi 8:7)

“kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.”

kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.

 Mungu kwa rehema yake ametoa mbadala wetu, yaani Yesu Kristo ambaye alikuja kulipa adhabu ya dhambi zetu kwa dhabihu yake msalabani. Hivyo kiini cha injili ni kifo cha Yesu, kuzikwa, na kufufuka na kupaa kwa Yesu Kristo. (1Kor.15:2-4).

Yatupasa tushikilie imara (Warumi 6:4-8)  injili ya kweli na ya  pekee. Mtume Paulo anasema kwamba injili ya kweli ni “nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa kila mtu aaminiye.” Anamaanisha kuwa wokovu haupatikani kwa jitihada za kibinadamu, bali kwa neema ya Mungu kupitia zawadi ya imani. (Waefeso 2:8-9). Sisi tunaomwamini na kumfuata Kristo, tumeokolewa na kupewa asili mpya (2Kor 5:17). 

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”

Moyo uliobadirika, tama mpya, mtazamo unaoonyeshwa katika matendo mema.

Wale waliookolewa kwa Nguvu za Mungu, daima wataonyesha ushindi wa wokovu kwa maisha yaliyobadilika. Tusiionee aibu kuihubiri injili. (Warumi 1:16).

“kwa maana siionei haya injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.”

Sisi yatupasa kuihubiri hii injili bila kuona haya ili kusudi mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu kwa watu wote utimilike.

Sisi yatupasa kuihubiri hii injili bila kuona haya ili kusudi mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu kwa watu wote utimilike.

 

Marejeo

1.Burridge,R.A.(2006), “Gospels” The Oxford handbook of Biblical studies, Oxford press.

2.Parker, D.C. (1997), The living text of the gospels, Cambridge, Cambridge University Press.

3.Morris Leon, (1986), New testament theology: Zondervan publishers.

4.Seccombe,D (2016), The gospel of the Kingdom, Cape Town : Whitefield publications.

LOAD MORE
Loading